KERO LA UTAPELI KATIKA ZOEZI LA UAJIRI WA WANAJESHI

KERO LA UTAPELI KATIKA ZOEZI LA UAJIRI WA WANAJESHI

Majeshi kote ulimwenguni mara kwa mara huwaajiri wanajeshi wapya kwa sababu tofauti. Mathalan, huenda pakawa na haja ya kujaza upungufu uliopo au haja ya kupata stadi maalum zinazohitajika kutokana na maendeleo ya kiteknolojia na changamoto za kiusalama za kisasa. Vilevile, uajiri hufanyika kufuatia upanuzi jeshini unaohitaji wanajeshi zaidi au katika juhudi za kukidhi mahitaji maalum ya kitaifa ama kujaza nafasi za wanajeshi walioaga au kustaafu.

Jeshi la Kenya sawia na majeshi mengineyo vilevile huwaajiri wanajeshi wapya kila mwaka na kwa kawaida huajiri katika vitengo sita tofauti: Kile cha Maafisa wa Majukumu-Jumla, yaani, General Service Officer (GSO) Cadets, Maafisa wa Majukumu-Jumla waliohitimu vyuoni; Graduate GSO Cadets, Maafisa wa Majukumu Maalum; Specialist Officers, Askari wa Majukumu-Jumla; General Duty Service Members, Askari wa Majukumu Maalum; Tradesmen/women huku cha mwisho kikiwa kile cha Askari Wazee, yaani, Constabularies.

Wanaoazimia kujiunga na Jeshi la Kenya ni sharti kutimiza mahitaji na kuwa na viwango vya elimu vihitajikavyo.

  • Wote wanahitajika kuwa wakenya bila uraia wa nchi nyingine,
  • kuwa na kitambulisho halisi cha mwananchi wa Jamhuri ya Kenya na wawe kati ya miaka 18 hadi 26 ikiwa ni Maafisa na Askari wa Majukumu-Jumla.
  • Askari wa Majukumu Maalum lazima wawe na vyeti au nyaraka za kiserikali zinazoashiria ustadi wao katika nyanja tofauti.
  • Maafisa na Askari wa Majukumu Maalum wenye stashahada wasipitishe miaka 30 kisha makasisi na mashehe wasiwe na zaidi ya miaka 39.
  • Zaidi, wote wanahitajika kuwa na siha kulingana na viwango vinavyotakikana katika Jeshi la Kenya na kutokuwa na rekodi za uhalifu.
  • Maafisa na Askari wa kike hawatakikani kuwa na uja-uzito wakati wakiajiriwa.
  • Hatimaye, waliostaafu jeshini au kuhitimu katika Huduma ya Vijana kwa Taifa na wanaoazimia kujiunga na jeshi kama Askari Wazee wanahitajika kuwa kati ya miaka 30-55 na 35-45 mtawalia.
  • Waliostaafu lazima wamiliki vyeti vya kustaafu vinavyoashiria kwamba mienendo yao ilikuwa ‘Mizuri Sana.’

Uajiri huu ni zoezi lililo wazi sana na ambalo hujulishwa kwa umma kupitia vyombo vya habari na hali kadhalika mitandaoni. Hususan, hutangazwa kwenye gazeti la Daily Nation, The Standard, The Star na The People Daily, Redio ya KBC, runinga ya KBC na ile ya Citizen. Kwenye mitandao ya kijamii, zoezi hili hutangazwa kwenye mtandao wa Twitter katika @Kdfinfo na ule wa Facebook katika @OfficialKDF.

Licha ya umma kufahamishwa kwa mapana na marefu kuhusu zoezi hili na kadhalika kutahadharishwa dhidi ya matapeli, kila mwaka Jeshi limezidi kupata malalamishi kwamba wananchi wametapeliwa kila kilicho chao katika juhudi za kupata uajiri wa wapendwa wao. Jeshi linakiri kwamba wanaohusika katika utapeli huu huwa ni raia na vilevile visa vya wanajeshi wapotovu kuhusika vimekuwepo. Hata hivyo, wanajeshi wahusikao na kutambulika, bila shaka hujutia vitendo vyao kwani hushtakiwa kwenye mahakama ya kijeshi, yaani, Court Martial, na wakati wote hupoteza kazi na zaidi kufungwa kwenye magereza ya kiraia.

Katika zoezi la uajiri la mwaka wa 2021 kwa mfano, palikuwepo na takribani visa vinane vya utapeli ambavyo vilihusisha maafisa wanane na askari thelathini na watano. Kati ya askari hao matapeli, kunao tayari walikuwa wamestaafu na hivyo kesi zao zinaendeshwa katika mahakama za kiraia. Kwa wale maafisa na askari ambao bado walikuwa kazini, kesi zao ama zinaendelea katika mahakama ya kijeshi au wamekwishapigwa kalamu na kufungwa kwenye magereza ya kiraia baada ya kesi zao kuamuliwa.
Matapeli kila siku wanabuni namna tofauti za kuwalaghai Wakenya waso hatia. Baadhi ya hila ambazo wametumia katika siku za hivi majuzi ni pamoja na kufanya matangazo sambamba kwenye mitandao ya kijamii huku wakitoa anwani za barua pepe na nambari za simu mbadala, kuunda akaunti kwenye mitandao ya kijamii wakitumia picha au majina ya viongozi wa kijeshi na wale wa kitaifa huku wakijidai kuwasaidia raia wema kupata uajiri jeshini na hali kadhalika kupiga simu au kutuma jumbe za simu na kuwaandikia barua pepe Wakenya huku wakijidai kuwapa ‘usaidizi’ katika zoezi linaloendelea. Wengine wameandaa barua za mwaliko ambazo wanawauzia Wakenya huku wakijitambulisha kama wasaidizi wa Mkuu wa Majeshi (Chief of the Defence Forces) au wafanyikazi wa Ikulu. Zaidi, kuna wale wanaoshawishi kwamba wana uwezo wa kuchapisha nakala za barua za mwaliko huku wengine wakidai wana uhusiano na timu za uajiri nyanjani au kudanganya kwamba Jeshi linaajiri ili kuziba mianya iliyoachwa na wanajeshi fulani wasioweza kukamilisha mazoezi katika vyuo vya kijeshi vya mafunzo.

Makala haya yameandikwa kwa lugha ya Kiswahili, lugha ya taifa, ili kuifikia hadhira-lengwa pana zaidi na kuitahadharisha kwa mara nyingine dhidi ya kutoa au kuchukua milungula katika zoezi zima la uajiri wa wanajeshi linaloendelea mwezini Agosti na Septemba, 2023. Vigezo vilivyokwisha orodheshwa katika makala haya ndivyo vinavyohitajika katika zoezi hilo na wala sio hela!
Wakenya wote wanahimizwa kuripoti visa vya utapeli kupitia nambari za rununu 0726419706/0726419709. Vilevile, visa vinaweza kuripotiwa kupitia anwani ya barua pepe publicaffairs@mod.go.ke na visa hivyo vitashughulikiwa ipasavyo.

Tunawatakia heri wote wanaostahili vitengo tofauti katika zoezi linaloendelea la mwaka wa 2023 ambalo bila shaka linazidi kutangazwa kupitia vyombo vya habari vya kitaifa na hali kadhalika kwenye mitandao ya kijamii ya Jeshi letu.

Jeshi zaidi linasema shukrani kwa wote walioripoti visa vya ufisadi na utapeli hapo awali na hivyo kuwezesha uchunguzi uliofanikisha mashtaka ya watenda-maovu.

Add Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

X-Frame-Options: SAMEORIGIN
Skip to content